Magazeti ya Ijumaa Januari 21, 2022 yanaangazia kukamilika kwa kesi ya BBI katika mahakama ya Upeo Alhamisi Januari 20.
Sasa Jaji Mkuu Martha Koome anatarajiwa kuongoza mahakama hiyo katika kutoa uamuzi kuhusu hatma ya BBI.
People Daily
Gazeti hili lina taarifa kuhusu kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi ambaye atafanya mkutano wa wajumbe wa chama chake Jumapili Januari 23.
Mudavadi ameahidi Wakenya kutakuwa na tangazo kubwa ambalo litatikisa ulingo wa kisiasa katika safari ya kuingia Ikulu mwezi Agosti.
Aidha, kuna taarifa pia kuhusu amri ya Rais Uhuru Kenyatta kuwa biashara ya vyuma vikuukuu isitishwe mara moja. Kenyatta alisema biashara hiyo inatumika na wahalifu kuharibu mali ya umma ambayo imegharimu mamilioni kuundwa.
Alitaka sheria maalum ya kuhusiana na biashara hiyo kuundwa kabla ya kurejelewa.
The Star
Gazeti la The Star lina taraifa kuhusu siasa za uchaguzi wa urais ambapo inaarifiwa kinara wa ODM Raila Odinga amejipanga pakubwa kuhakikisha anaingia Ikulu.
Magavana ambao wanamuunga mkono Raila watakuwa wanaripoti kwa bodi na mwenyekiti wa kamati za kaunti zinazompangia kazi.
Daily Nation
Gazeti hili linasema Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kufanya mageuzi serikalini baada ya baadhi ya mawaziri kumpa notisi ya kuondoka.
Mawaziri hao wanapanga kuingia kwenye ulingo wa siasa kuwania nyadhifa mbalimbali na hivyo ni lazima Rais apange nyumba yake upya.
Taifa Leo
Taarifa hapa ni kuhusu masaibu ambayo yanaendelea kumwandama naibu rais William Ruto katika kesi mahakamani Hague.
Inaarifiwa sasa imeibuka kuwa Meshak Yebei alikuwa ni mmoja wa waliokuwa wakipanga jinsi ya kusambaratisha kesi ya DP Ruto iliyokuwa ikiendelea The Hague.
Baadaye aligeuka na kuwa mmoja wa mashahidi waliokuwa wameratibiwa kufika mbele ya mahakama hiyo ili kutoa ushahidi dhidi ya DP Ruto na mtangazaji Joshua Arap Sang.
Alitoweka mnamo Disemba 2014 kabla ya mwili wake kupatikana katika mbuga ya Tsavo ukiwa na majeraha mabaya.
Wakili Paul Gicheru ambaye alijisalimisha kwa ICC baada ya kushtakiwa kwa kuhusika katika kusambaratisha kesi ya DP Ruto alisema walikuwa wamekutana na Yebei kupanga vile kesi hiyo itaanguka.
Collins Oluyali is a popular columnist who reviews the Kenyan dailies every morning in the Magazetini section, giving it a political angle with facts weaved in rich Kiswahili. Collo is also a strategist in the WKT team.