UN yalaani shambulio hatari la angani katika gereza la Yemen
Picha | BBC

UN yalaani shambulio hatari la angani katika gereza la Yemen

  • Na BBC

Umoja wa Mataifa umelaani shambulizi la anga dhidi ya kituo kimoja cha mahabusu nchini Yemen na kuua zaidi ya watu 70.

Kituo hicho kilichopo katika mji wa Saada, ambao ni ngome ya waasi wa Kihouthi kaskazini -magharibi mwa Yemen, kilishambuliwa siku ya Ijumaa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika taarifa yake alisema kwamba “makabiliano yanapaswa kukomeshwa”.
Katika taarifa siku ya Jumamosi, muungano unaongozwa na Saudi Arabia – kupigana na waasi wa Houthi nchini humo walipinga kutekeleza shambulio hilo la angani.

Muungano huo pia ulisema eneo hilo liko katika orodha ya maeneo ambayo hayapaswi kushambuliwa kama ilivyofikiwa katika makubaliano na Umoja wa Mataifa na haikuwa imeripotiwa na shirika la Msalaba mwekundu.
Vikosi vya muungano vinavyoongozwa na Saudia-vimekuwa vikipigana na waasi wa Houthi tangu mwaka 2015. Maelfu ya raia wakiwemo zaidi ya watoto 10,000, wameuawa na wengine kujeruhiwa kutokana na ashambulio ya moja kwa moja katika vita hivyo.

Mamilioni ya watu wanasemekana kusambaratishwa na watu wengi wanakabiliwa na tishio la njaa.
Saa kadhaa baada ya shambulio la angani, wahudumu wa uokozi bado wanatoa miili kwenye vifusi, huku matumaini ya kupata manusura ikiendelea kudidimia, anasema mwandishi wa BBC Mashariki ya Kati, Anna Foster.

Idadi kamili ya waliofariki haijabainika. Médecins Sans Frontières (MSF)linasema karibu watu 70 waliuawa, ijapokuwa idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka.
Televisheni inayoendeshwa na Wahouthi ilionyesha wanaume wakiondoa vifusi kwa mikono yao katika eneo la tukio na waliojeruhiwa wakiwa hospitali ya eneo hilo. MSF ilisema hospitali moja imepokea zaidi ya majeruhi 200.

Share this article

Comments

No comments yet. Why don’t you start the discussion?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *