
Isaac Juma is said to have been murdered as a result of family land dispute/Courtesy
Simanzi imeghubika kijiji cha Rukaya, Mumias Magharibi katika kaunti ya Kakamega baada ya shabiki maarufu wa soka Isaac Juma kuripotiwa kuuawa kinyama nyumbani kwake.
Inasemekana Juma aliuawa jana mwendo wa saa tano usiku baada ya kuvamiwa na genge la watu waliokuwa wamejihami, kwa mujibu wa mkewe Farida, aliyeongezea kuwa hili lilitokana na mzozo wa ardhi.
“Tulikuwa tunakula chajio kabla ya kusikia kondoo wakilia nje. Alipotoka kwenda kutazama, nilisikia mayowe. Nilipomfuata, niligutuka kuona mume wangu akipiga nduru huku waliomteka wakimkatakata jinsi ng’ombe huchinjwa,” Bi. Farida alihadithia wanahabari.
Bi. Farida alisema mumewe alikuwa amemdokezea kuwa akifariki katika hali tata basi itakuwa ni kwa sababu ya mzozo wa ardhi. Polisi wanasema hakika kisa hicho kinaashiria mzozo wa ardhi.

OCPD wa Mumias Magharibi Stephen Muoni alithibitisha tukio hilo na kusema kuwa washukiwa wawili wamekamatwa kutokana na kifo hicho huku uchunguzi wa kutafuta wengine ukiendelea.
“Alikuwa ndani ya nyumba aliposikia mvutano nje na alipotoka yeye, mwanawe na nduguye walivamiwa ghafla na wanaume wawili, akauawa huku nduguye na mwanawe wakifanikiwa kutoroka,” OCPD alisema.
Mwendazake alikuwa muuzaji wa magazeti na shabiki wa moyoni wa AFC Leopards (Ingwe) na Harambee Stars.
Mwaka wa 2011, Juma alipata tuzo la Chairman’s Lifetime Achievement Award (KPL FOYA) kwa mchango wake wa ushabiki.
Ameacha nyuma watoto 10, wake wawili huku mwili wake ukihifadhiwa katika hifadhi ya maiti ya Butere Hospital.


Tom Lutali is a seasoned scribe based in Lugari Sub-County in Kakamega County who writes human interest stories and sports for WKT.
1 thought on ““Alichinjwa nikitazama:” Mkewe Juma, shabiki sugu wa Stars na Ingwe, asimulia”