Huku kipute cha AFCON 2021 kikielekea kilele, wenyeji Cameroon wamejikatia tiketi ya nusu fainali baada ya kuwafunga limbukeni Gambia 2-0.
Licha ya mechi hiyo kuisha 0-0 kipindi cha kwanza, mambo yalibadilika kipindi cha pili na Cameroon wakafunga Gambia 2-0 ndani ya dakika 15 za kwanza.
Toko Ekambi aliwafungia wenyeji mabao yote mawili dakika ya 50′ na 57′.
Kwa sasa Cameroon watasuburi mshindi kati ya Morocco na Misri ambao wanacheza leo.
Ushindi wa Burkina Faso
Kwingineko, Burkina Faso waliwaduwaza Tunisia 1-0. Burkina Faso walipata bao lao la pekee kupitia mshambulizi Dago Ouattara dakika ya 46, kipindi cha kwanza. Hata hivyo, mchezaji huyo alipata kadi nyekundu dakika ya 82′ baada ya kucheza visivyo.
Kipute cha leo
Leo, wajukuu wa Pharaoh, Misri, watakuwa wanacheza na Morocco kwenye debi la Waarabu. Ni mechi ambayo imekisiwa kuwa ngumu sana katika michuano hii ya AFCON.
Senegal nao watakuwa wanatarajia kuvuna katika nne bora watakapowaalika limbukeni Equatorial Guinea leo saa nne usiku.
Mshindi kati ya Morocco ama Misri atakutana na wenyeji Cameroon na mshindi kati ya Senegal na Equatorial Guinea atakutana na Burkina Faso.
Tom Lutali is a seasoned scribe based in Lugari Sub-County in Kakamega County who writes human interest stories and sports for WKT.