Baadhi ya taarifa kwenye magazeti ya Ijumaa Februari 4 ni ripoti kuwa rais Uhuru Kenyatta anaanza kikao cha siku mbili na wabunge wa Jubilee katika Ikulu.
Taarifa nyingine ni kuhusu hisia mseto ambazo umeibuka baada ya serikali kupendekeza mswada wa kubadili sheria kuhusu uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti.
People Daily
Taarifa kuu hapa ni kuhusu mageuzi ya sheria ya uchaguzi yanayopendekezwa na upande wa serikali Bungeni.
Kiongozi wa Wengi Amos Kimunya alipendekeza mswada wa kufanyia mabadiliko sheria ya uchagizi ili kusiwe na upeperushaji wa matangazo moja kwa moja kupitia runinga mwezi Agosti, miongoni mwa mageuzi mengine.
Naibu Rais William Ruto amekashifu hatua hii akisema ni hatari sana na huenda ikasababisha mzozo kuhusu uchaguzi ujao. Alitaja hatua hiyo kama njama ya kujaribu kuvuruga matokeo ya uchaguzi ili kuhakikisha mgombea fulani anashinda uchaguzi huo.
“Juhudi za kujaribu kulazimisha Wakenya project kitendawili kwa kutumia kifua na mbinu zisizo za kisheria ni hatari kwa taifa,” alisema DP.
Spika Justin Muturi na Musalia Mudavadi pia walisema hatua ya serikali inazua wasiwasi kuwa kuna njama ya wizi katika uchaguzi huo.
The Star
Gazeti hili linasema kuwa kinara wa ODM Raila Odinga amechukua likizo kutoka kampeni na anatarajiwa kusafiri nje ya nchi kwa siku kumi.
Raila anafunga safari kuelekea Ethiopia na India ambapo atajituliza baada ya kufanya misururu ya mikutano kuhusu Azimio la Umoja.
Bwana Raila amekuwa katika eneo la Mlima Kenya ambapo alifanya mikutano Murang’a, Thika na Nyandarua kurai wakaazi kumuunga mkono. Alimalizia kaunti ya Kajiado na kwa siku kumi sasa atakuwa akipunga hewa kule mjini Addis na New Delhi.
Aidha, gazeti hili lina taarifa pia kuhusu mswada ambao unapendekezwa kuhakikisha waajiri hawawapi wafanyakazi kibarua wakiondoka kazini. Mswada huo utafanya iwe kinyume cha sheria kwa mfanyakazi kupewa kibarua nje ya saa za kazi ambazo huwa kati ya saa mbili asubuhi na saa kumi na moja jioni.
Collins Oluyali is a popular columnist who reviews the Kenyan dailies every morning in the Magazetini section, giving it a political angle with facts weaved in rich Kiswahili. Collo is also a strategist in the WKT team.