Magazeti ya Jumanne, Februari 8, yameangazia ishara za rais Uhuru Kenyatta kuwa atamuunga mkono kinara wa Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga katika uchaguzi wa Agosti 9.
Magazeti haya pia yanaripoti kuhusu mipango ya muungano unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto, Kenya Kwanza kufutilia mbali mtaala mpya wa elimu wa Umilisi na Utendaji(CBC) ukitwaa mamlaka.
Daily Nation
Katika gazeti hili, Rais Uhuru anatarajiwa kumuidhinisha rasmi Raila kuwa mgombea wa urais.
Uhuru pia anatarajiwa kuweka wazi ramani ya mrithi wake katika kongamano lijalo la kitaifa la wajumbe wa chama cha Jubilee.
Siku ya Jumatatu, Februari 7, Uhuru aliwaonya wanaompinga pamoja na muungano wa Azimio La Umoja kujiandaa kwa kivumbi kikali akimkashifu Ruto kwa kumpaka tope badala ya kuchapa kazi.
Taifa Leo
Viongozi kutoka muungano wa Kenya Kwanza wamejipata pabaya baada ya kutangaza mipango ya kufuta mtaala mpya wa elimu wa Umilisi na Utendaji (CBC) wakitwaa mamlaka.
Wakiongozwa na kinara wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, walisema watafutilia mbali CBC ili kumaliza sintofahamu katika sekta ya elimu.
Lakini katibu mkuu wa Chama cha Walimu (KNUT), Collins Oyuu, aliwaonya wanasiasa dhidi ya kucheza karata na CBC.
Mfumo wa CBC unalenga kuwaandaa na kukuza talanta ya wasomi wakiwa wangali wachanga.
The Standard
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imerekodi idadi ndogo zaidi ya wapiga kura katika zoezi tatu ya usajili.
IEBC ilifaulu kuwasajili wapiga kura wapya 1,031,645 pekee katika awamu ya pili iliyofunga jamvi siku ya Jumapili, Februari 6.
Tume hiyo inayoongozwa na Wafula Chebukati ilikuwa inalenga kuwasajili wapiga kura milioni sita katika awamu ya kwanza na wengine 4.5 milioni katika awamu ya pili.
Idadi hiyo ni ndogo zaidi ikilinganishwa na ya kura ya maoni mwaka 2010, na chaguzi za 2013 na 2017
The Star
Kulingana na The Star, Kenya inapania kushabikia Uganda na Tanzania kupiga marufuku mifuko ya plastiki.
Haya yanajiri huku serikali ikisema sheria hiyo inatekelezwa kwa asilimia 95%. Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA), Mamo Mamo, alisema mamlaka hiyo imeweka sheria mbalimbali za kuzuia plastiki zilizopigwa marufuku kitaifa na kikanda.
Mamo alisema marufuku hiyo katika ngazi za ukanda yatatekelezwa na usaidizi wa mkurugenzi mkuu wa mataifa ya ukanda wa Afrika Mashariki.
Collins Oluyali is a popular columnist who reviews the Kenyan dailies every morning in the Magazetini section, giving it a political angle with facts weaved in rich Kiswahili. Collo is also a strategist in the WKT team.