
Wakaazi wa Likuyani wakishuhudia utafutaji wa miili ya ndugu wawili waliozama [Picha-West FM]
Biwi la simanzi limetanda katika kijiji cha Mmbasu katika kaunti ndogo ya Likuyani, Kakamega, baada ya msichana wa miaka 13 na nduguye wa miaka 12 kuzama maji Mto Kipsangui.
Kulingana na Andriano Limisi, amu yao, watoto hao waliondoka kwao asubuhi kwenda kucheza kwa jirani kabla ya kuelekea mtoni kuogelea.
“Waliondoka mwendo wa saa nne asubuhi kwenda kucheza. Mwendeshaji pikipiki ndiye aliyetutaarifu kuwa kuna watoto wawili ambao walikuwa wametolewa majini. Nilipoenda kutazama nilishtuka kupata ni wapwa wangu, ” alisema Lumisi.
Akidhibitisha kisa hicho, naibu chifu wa kata ya Soy Bonivanture Lugado alisema watoto hao wawili ni wanafunzi wa shule ya msingi ya Nangili na walikuwa wamemtembelea nyanya yao Maria Shayi msimu wa mapumziko ya Aprili.
“Watoto hawa wanaishi na mama yao Nangili, kata ya Kongoni, na walikuwa wamemtembelea nyanya yao kabla ya kukutana na vifo vyao,” Lugado alisema.
Mkuu huyo amezishauri familia zinazoishi karibu na mito kuwa makini na wanao hasa msimu huu ambapo shule zimefungwa.
Miili ya watoto hao imechukuliwa na maafisa wa kituo cha polisi cha Likuyani na inahifadhiwa katika hifadhi ya maiti ya Kimbilio, kaunti jirani ya Uasin Gishu.

Tom Lutali is a seasoned scribe based in Lugari Sub-County in Kakamega County who writes human interest stories and sports for WKT.