Magazeti ya Jumatatu, Machi 28, yameangazia mawimbi katika mbio za urais kufuatia madai ya Rais Uhuru Kenyatta kwamba naibu wake William Ruto alipanga njama ya kumwondoa madarakani.
Katika majibu yake, Ruto alitaja madai ya Uhuru kama yasiyokuwa na msingi bali ni propaganda.
- The Star
Mawimbi yanapiga kinyang’anyiro cha urais kufuatia madai ya Uhuru. Alipokuwa akikutana na wazee wa jamii ya Agikuyu katika Ikulu ya Nairobi mnamo Jumamosi, Machi 26, rais alifichua njama ambayo naibu wake alipanga dhidi yake.
Uhuru alifichua kuwa naibu wake Ruto alipanga njama ya kumng’oa mamlakani mara tu baada ya kuchaguliwa kwa muhula wake wa pili na wa mwisho.
Rais anaripotiwa kumuelezea Ruto kama mwanasiasa mwenye tamaa ya madaraka aliyetaka kumpindua serikalini.
Hata hivyo, katika majibu yake, Ruto alipuuzilia mbali madai hayo akiyataja kuwa propaganda zisizo na msingi wowote.
“Tafadhali waepushe Wakenya na uongo na propaganda zisizo na maana. Huna ajenda. Tafadhali usiharibu nchi yetu kwa uongo usio na maana,” Ruto alinukuliwa na The Star akisema.
- Daily Nation
Gazeti hili linaripoti kuhusu ajali ambapo mfanyakazi alifariki kwenye tanuru katika kinu cha Thika cha Blue Nile.
Caleb Otieno, mwenye umri wa miaka 35, anasemekana kuangukia tanuru mnamo Ijumaa, Machi 26, akiwa kazini, wenzake wakisema kuwa mwili wake ulikuwa umeyeyuka kabisa.
Familia yake inashuku kuliwepo na mchezo mchafu licha ya polisi kudai ilikuwa ajali tu.
Viwango vya usalama vya kampuni hiyo vimezua shaka huku familia ikiiomba kampuni hiyo kuwajibikia ajali hiyo.
- The Standard
Gazeti la The Standard pia lilijikita katika mzozo uliopo katika kiti cha urais siku mbili baada ya Uhuru kufichua kuwa naibu wake alipanga njama ya kumng’oa mamlakani.
Naibu rais hata hivyo alipuuzilia mbali madai hayo akisema hajawahi kuwa na mawazo kama hayo.
Ruto alishangaa jinsi angekuwa na hila kama hizo ilhali alikuwa mstari wa mbele katika uchaguzi wa Uhuru na kuchaguliwa mara ya pili 2013 na 2017 mtawalia.
Alimsuta Uhuru ambaye alisema alikuwa akieneza uwongo na propaganda.
Collins Oluyali is a popular columnist who reviews the Kenyan dailies every morning in the Magazetini section, giving it a political angle with facts weaved in rich Kiswahili. Collo is also a strategist in the WKT team.