Magazetini: Shule za kibinafsi zatawala KCPE 2021

Magazetini: Shule za kibinafsi zatawala KCPE 2021

Magazeti yameangazia pakubwa matokeo ya KCPE 2021.

Magazeti ya Jumanne, Machi 29, yanaripoti kwamba mamilioni ya pesa zinazodaiwa kufichwa kisiri na matajiri zitatumika kununua vifaa vya COVID-19.

Magazeti haya pia yamegusia kuboreka kwa matokeo ya Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) baada ya mtahiniwa bora kupata 428.

  1. People Daily

Kulingana na chapisho hili, mamilioni ya pesa zinazodaiwa kuibwa na watu matajiri zaidi nchini Kenya zitarejeshwa nchini ili kununua vifaa vya COVID-19 kufuatia makubaliano ya kihistoria yaliyotiwa saini mjini London.

Makubaliano hayo na Jersey, kisiwa kinachojitawala Uingereza, yalisifiwa kama “ushindi kwa watu wa Kenya” na Balozi wa Kenya nchini Uingereza, Manoah Esipisu.

Mamlaka ya Jersy ilianza uchunguzi wa miaka tisa katika mamlaka 12 baada ya kubainika kuwa mali ya aliyekuwa mkurugenzi wa kampuni ya Kenya Power Samuel Gicheru ilikuwa ikifichwa kutokana na kesi ya talaka iliyomhusisha yeye na mkewe Salome Njeri.

Kama sehemu ya uchunguzi huo, mwaka wa 2011, Gichuru na aliyekuwa Waziri wa Fedha Chris Okemo walishtumiwa kwa kuchukua pesa kutoka kwa mashirika ya kimataifa ambayo yalitumwa kwa kampuni iliyosajiliwa Jersey.

  1. Daily Nation

Gilgil Hills Academy ilitoa mtihaniwa bora wa KCPE 2021 huku ikisajili idadi kubwa ya watahiniwa waliozoa zaidi ya alama 400 katika kipindi cha miaka sita.

Magata Bruce Mackenzie aliibuka mtahiniwa bora kitaifa kwa kupata alama 428, akifuatiwa kwa karibu na Momanyi Ashley Kerubo wa shule ya Makini aliyekuwa na alama 427.

Darasa la mwaka wa 2021 lilikuwa na watahiniwa 11,857 waliopata alama 400 na kuendelea.
Mwaka wa 2018 pekee ndio uliandikisha idadi kubwa wakati watahiniwa 12,273 walipata zaidi ya alama 400 kati ya jumla ya 500.

  1. Taifa Leo

Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kimefichua kuwa idadi ya wanasiasa watakaopewa tikiti ya moja kwa moja ya kuwania viti tofauti katika uchaguzi wa Agosti itaongezeka siku zijazo.

Mwenyekiti wa ODM tawi la Mombasa, Mohammed Khamis, alipuuzilia mbali watu wanaopinga hatua ya chama hicho akisema kuwa katiba ya chama hicho inatambua hatua hiyo.

Katika eneo la pwani, ODM inatarajiwa kukabidhi tikiti za bwerere kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Kilimo Hamadi Mboga, anayetaka kuwania kiti cha ugavana wa Kwale, wabunge Mishi Mboko (Likoni) na Badi Twalib (Jomvu).

Hata hivyo, Khamis alisema kuwa chama hicho kinachoongozwa na Raila Odinga pia kitazingatia umaarufu wa mgombeaji kabla ya kupewa tikiti za moja kwa moja.

  1. The Standard

Vuguvugu la Azimio La Umoja limemtaka Naibu Rais William Ruto kukoma kumhusisha kinara wake Raila na mpango uliofichuliwa wa kumtimua Rais Uhuru Kenyatta.

Akizungumza mjini Kakamega akiandamana na Raila mnamo Jumatatu, Machi 28, aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth alisema madai ya Uhuru kwamba Ruto alitaka kumng’oa mamlakani ni ya kweli.

Kenneth alisema ni lazima makamu wa rais ashughulikie suala hilo bila kumtaja Raila.

Uhuru, akihutubia wazee wa Mlima Kenya Jumamosi, Machi 26, baada ya kumtembelea Ikulu ya Nairobi, alisema hataunga mkono azma ya urais ya Ruto kwa sababu alitaka kumwondoa madarakani.

  1. The Star

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko anatarajiwa kurejea katika siasa za jiji kufuatia kutimuliwa kwake ofisini mwaka 2020.

Sonko, wiki jana alijiunga na Chama cha Wiper, huku duru zikisema anajiandaa kurejea katika siasa za jiji.

Kulingana na msaidizi wa gavana huyo wa zamani Francis Wambua, Sonko atakuwa akijaribu kurejesha kiti chake cha ugavana.

Mapema mwezi huu, Sonko alijiuzulu kutoka kwa Chama cha Jubilee kwa madai kwamba aliondolewa afisini kinyume cha sheria chini ya uongozi wa Uhuru.

Share this article
Leave a Comment

Comments

No comments yet. Why don’t you start the discussion?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *