
Mwanamke mmoja Bungoma amevumbua ajira inayokimu wanawake 40. (Picha- Tom Lutali, WKT)
Licha ya kupevuka kwa kizazi cha sasa, wengi wa wanawake bado wamefungwa na mila na desturi potovu za jamii. Aghalabu, itikadi hizi zimefanya mtoto wa kike kusalia nyuma dunia nzima ikipiga hatua.
Kwa mujibu huo, makala ya leo yamamuangazia Mama Anastasia Waswani Ong’eti ambaye, katika ukakamavu wake, amevumbua ajira ya kusaidia wanawake wenzake kukikimu.
Mama huyu anaendeleza mradi wa ushonaji nguo na karakana yake inayositiri wanawake 15 inapatikana kaunti ndogo ya Kanduyi, kaunti ya Bungoma katika barabara kuu ya Kanduyi-Bungoma mkabala na chuo cha mafunzo ya udaktari cha KMTC.
Tom Lutali anazungumza naye.

Je, haya yote yalianza vipi?
Kazi hii niliibuni baada ya kuachia shule kidato cha pili kisha baba akaniambia niende nisome ushonaji Nairobi kule Industrial Area. Nikamaliza, nikafuzu na kuenda Mombasa kufungua kibanda na nikakaa huko kwa miaka saba.
Wakati huo nilikuwa na tumaini kuwa nitafungua biashara kubwa ndipo nikaja hapa Bungoma nakafungua hili duka. Nimekaa hapa kwa muda wa miaka kumi.
Msukumo uliokufanya uanze mradi huu ni upi?
Nilipokuwa katika ndoa, nilikuwa na changamoto nyingi sana na nikaona ni heri kuanzisha kikundi ili kusaidia akina mama kukuza talanta zao za kutumia mikono yao na akili kutoa ufukara.
Hapa mnashughulika na nini hasa?
Tunashona vitambaa, nguo za shule, za harusi na za kukupambia nyumba na kila aina ya nguo.
Tangu uanzishe mradi huu akina mama wangapi wamefuzu?
Tangu nianzishe mradi huu zaidi ya akina mama 40 wamefuzu. Kumi kati yao wamefungua maduka yao na wanaendeleza biashara zao.
Uhusiano wako na akina mama wenzako hapa ni vipi?
Uhusiano wetu nao ni mwema kabisa. Wao hunipatia sababu ya kutia bidii kila wakati.
Unajivunia nini kutokana na kazi yako?
Najivunia hii kazi maana imenisaidia kusomesha binti zangu watatu. Wawili kati yao wamefuzu kutoka vyuo vikuu na wa mwisho yuko mwaka wake wa mwisho sasa.
Pili, kupitia ajira hii nimesaidia ndugu zangu na kununulia babangu dawa kila mwezi kwa miaka miwili.
Tatu, nalisha familia yangu yote maana hata mume wangu kazi ilisimama.
Hii kazi inaathiri vipi maisha yako ya kila siku?
Kwa kweli, kama mwanamke, imeniathiri pakubwa– ninakosa kufanya majukumu ya nyumbani kama kupika. Nakosa pia kuenda kanisani maana naingia kazini saa moja asubuhi na kutoka saa moja jioni.
Changamoto unazokumbana nazo katika kazi yako?
Changamoto ni kuwa nyumba hii ni ndogo ikikumbukwa kuwa nina akina mama 15 hapa. Pili, ni gharama ya kulipa kodi ya nyumba na tatu ni ukaidi wa wateja wanaolipia nguo pesa kiasi lakini hawarudi kumalizia agano.


Tom Lutali is a seasoned scribe based in Lugari Sub-County in Kakamega County who writes human interest stories and sports for WKT.