
Magazeti ya Jumanne, Mei 24, yanaripoti namna kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka yuko njia panda baada ya chama chake kumtaka arejee katika muungano cha Azimio la Umoja siku chache baada ya kutangaza azma yake ya urais.
Magazeti haya pia yamegusia mkutano ambao Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeitisha na wagombeaji urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.
- The Standard
Kulingana na gazeti hili, vyama tanzu vya Kenya Kwanza Alliance vilimkosoa Naibu Rais William Ruto na mgombea mwenza wake Rigathi Gachagua kwa kuwataka wapiga kura kuwachagua wagombeaji wa UDA pekee.

Mwenyekiti wa Chama cha Farmers of Kenya, Irungu Nyakera Nyakera, ambaye pia ni mmoja wa vinara wa Kenya Kwanza, alisema ananusia uovu katika hatua hiyo.
- People Daily
Gazeti la People Daily linaripoti kuwa mgombea urais Raila Odinga alisema kanisa litakuwa na nafasi muhimu katika kusimamia masuala ya nchi iwapo atashinda uchaguzi wa Agosti 9.
Raila alisema anatambua jukumu muhimu la viongozi wa kidini katika kudumisha amani na utangamano nchini.

Kiongozi huyo wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya alisema atatafuta ushirikiano na makasisi katika masuala ya utawala na usalama.
Raila aliwaomba makasisi kukumbatia na kuhubiri amani kabla ya uchaguzi wa Agosti 9 na kufikia makanisa huru kuunga mkono azma yake ya urais.
- Taifa Leo
Kulingana na chapisho hili, mwanamume aliyevunja ofisi ya Nairobi Chapel kwenye Barabara ya Ngong na kuiba kipatakilishi na vifaa vya thamani ya KShs 110,000 atafungwa jela miaka mitatu na nusu.
Joseph Kamau Ndung’u alipewa adhabu hiyo na hakimu mkuu mwandamizi Esther Bhoke wa mahakama ya Kibera. Alinyimwa uhuru wa kulipa faini.
Bhoke alisema ripoti ya muda wa majaribio iliyowasilishwa mbele yake haikumpendelea Ndung’u kupewa hukumu ya kutozuiliwa. Ndung’u alikiri kuvunja kontena kanisani na kutekeleza wizi huo baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapili katika kanisa hilo.
Aliiba kipatakilishi na mali ya thamani ya Rodgers Koome Kinyua ambaye ni fundi wa sauti katika kanisa hilo. Ndung’u pia aliiba KShs 200 na mwavuli ambao Kinyua alikuwa ameuweka kwenye begi ya kipatakilishi hicho.
4. Daily Nation

Chapisho hili linaripoti kwamba mawaziri, magavana na wabunge wanaongoza timu ya watu 16 kote nchini ambao ni sehemu ya kikosi cha kampeni ya Raila Odinga.
Muungano wa Azimio la Umoja umepanga nchi katika mikoa kumi na sita huku timu za wanachama wasiopungua sita zikiwa zimesambaa.
Raila Odinga na mgombea mwenza wake, kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua, wanaongoza timu ya urais ikiwa na wanachama kumi na mmoja, hasusan wanachama wa Jubilee na ODM.
Muungano huo pia umeunda timu tatu za wanawake na mbili za vijana zilizosambaa kote nchini.
“Katika azma ya Kenya hii mpya, nimeandaa programu ambayo ninaamini itatimiza ndoto zetu. Kwanza nimeunda miundo 12 ili kuendesha kampeni ya Azimio,” Raila alisema.
- The Star

Gazeti hili linaripoti kuwa maelezo mapya yameibuka kuwa upeperushaji wa matokeo ya uchaguzi wa urais unaweza kushindikana tena katika baadhi ya vituo wakati wa uchaguzi wa Agosti 9.
IEBC ilisema kuwa angalau vituo 1,100 vya kupigia kura bado havijaunganishwa kwenye mtandao wa 3G, hivyo basi kushindwa kuwasilisha matokeo.
Akihutubia wanahabari baada ya kukutana na wawaniaji urais katika eneo la Bomas of Kenya jijini Nairobi, mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebutaki alisema kuwa ripoti kutoka kwa Mamlaka ya Mawasiliano ilionyesha kuwa vituo hivyo visivyo na mtandao huenda visiweze kuwasilisha matokeo kwenye kituo cha kitaifa cha kujumilisha kura.
“Tuliwaomba ripoti ya ubora wa huduma wakasema vituo 1,100 havina 3G. Walituomba tufanye majaribio ili kuangalia ikiwa inawezekana kusambaza mtandao wa kasi ya chini,” Chebukati alisema.
Kituo cha kupigia kura kinajumuisha vituo kadhaa, na vituo 1,100 vinaweza kuhusisha maelfu ya wapiga kura.
Chebukati aliwahakikishia Wakenya kwamba hakutakuwa na hitilafu yoyote itakayosababisha kushindwa kwa vifaa vya kukagua fomu na kutuma matokeo Nairobi

Collins Oluyali is a popular columnist who reviews the Kenyan dailies every morning in the Magazetini section, giving it a political angle with facts weaved in rich Kiswahili. Collo is also a strategist in the WKT team.