- Na Dennis Avokoywa
Mkulima mmoja kaunti ya Kakamega anakadiria hasara baada ya mifugo wake kuvamiwa kwa kukatwakatwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo.
Zaidi ya ng’ombe wanne walikatakatwa kwenye uvamizi huo uliotokea katika kijiji cha Shikungula eneo bunge la Shinyalu.
Kulinga na Anthony Muyonga, mkulima, anasema aligutushwa kutoka usingizini na kelele kutoka kwa boma la mifugo wake.
“Nilitaka kujua kilichokuwa kikijiri, ng’ombe walikuwa nje, walikuwa wamelala chini huku wakitokwa na damu,” alisema.
“Huenda nia yao ilikuwa kuwaiba ila wakashindwa,” aliongezea.
Ngombe hao walikuwa wamekatakwatwa miguuni na mgongoni; wengine wakiwa na alama za panga kichwani.
Akidhibitisha kisa hicho, naibu chifu wa eneo hilo Catherine Nelima alisema tiyari wameanzisha uchunguzi huku akiwarai wakaazi dhidi ya kujichukulia sheria mikononi mwao iwapo wametofautiana.
“Tumeanzisha uchunguzi kubaini wahusika. Ni vyema kusuluhisha migogoro kwa njia za kidiplomasia mbali na kujichukulia sheria mikononi,” alisema.
Kisa sawia na hiki kilitokea majuma kadhaa yaliyopita eneo bunge la Lugari kaunti hiyo hiyo ambako zaidi ya ng’ombe 10 walikatakatwa usiku.
Visa hivi vimekashifiwa vikali na wakaazi katika kaunti hiyo wakiwanyoshea maafisa wa usalama kidole cha lawama kwa kuzembea kazini na kuwa chanzo cha visa hivyo.
“Ingelikuwa ni pombe inapikwa hapa wangekuwa wamefika mara kadhaa. Tunataka maafisa hawa kubadilishwa,” alisema Nicholas Lukwa, mkaazi wa kijiji cha Shikungula.
Discover the pulse of Western Kenya with WKT – your go-to digital media platform for real-time updates, rich perspectives, and powerful stories that matter.