
Ukurasa wa mbele wa gazeti la Daily Nation [Picha-Hisani]
Magazeti ya Jumanne, Agosti 16 yameangazia pakubwa kutangazwa kwa William Ruto kuwa rais mteule licha ya ushindi wake kupingwa na makamishna wanne wa Tume Huru ya Uchaguzi(IEBC).
Magazeti haya pia yamegusia namna mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati, alistahimili vitisho na vurugu alipokuwa akimtangaza mshindi wa uchaguzi wa urais wa Jumanne, Agosti 9.
Daily Nation
Kulingana na gazeti hili, vinara wa muungano wa Azimio La Umoja One Kenya wamedokeza kuwa watakwenda mahakamani kukosoa matokeo ya urais yaliyotangazwa Jumatatu, Agosti 15.
Akivunja kimya chake baada ya Ruto kutangazwa rais mtele, mgombea mwenza wa Azimio Martha Karua alidokeza kuhusu kwenda kortini.
Msemaji wa muungano huo Makau Mutua naye alisema tangazo la Chebukati ni batili.
The Standard

Gazeti hili linaripoti kuwa ngumi na makonde yalitanda katika ukumbi wa Bomas huku makamishna wanne wa IEBC wakimuwacha Chebukati mataani na kufanya mkutano wao katika hoteli ya Serena wakijitenga na matokeo hayo.
Hata hivyo, Chebukati alionyesha ukakamavu na ujasiri akifichua kwamba alikuwa amesukumiwa presha ya kumtangaza mtu ambaye hakuwa mshindi lakini aliamua kufuata sheria kumtangaza Ruto rais wa tano wa Kenya.
“Najivunia kuwa huu ni uchaguzi wangu wa mwisho kusimamia lakini watakaokuja baada yangu watapata taasisi huru,” alisema Chebukati
Katika taarifa yake, Chebukati alisisitiza kuwa Wakenya walipiga kura na alikuwa na wajibu wa kutangaza matokeo ambayo yaliaoana matakwa ya wananchi.
Taifa Leo

Taifa Leo linaripoti kuwa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kenyatta Paul Wainaina amefutwa kazi rasmi.
Kaimu Naibu Chansela Wacheke Wanjohi alisema katika ujumbe kwa wafanyakazi wa chuo hicho na wanafunzi kuwa mawasiliano yoyote au maelekezo kutoka kwa Wainaina ni batili.
Wainaina alifutwa kazi mara ya kwanza Julai 12, kufuatia mvutano kati yake na serikali kuhusu kipande cha ardhi ambacho kilikuwa kimetengewa maendeleo. Siku kadhaa baadaye, Wainaina alipewa ahueni ya muda baada ya mahakama ya Ajira na Mahusiano ya Leba kuamuru arejeshwe kazini.
People Daily

Gazeti hili linaripoti kuwa vurugu ilizuka mjini Kisumu siku ya Jumatatu, Agosti 15, baada ya Ruto kutangazwa rais mteule.
Chebukati alimtangaza Ruto na mgombea mwenza wake Rigathi Gachagua kuwa rais na naibu rais mteule mtawalia. Punde baada ya tangazo hilo, maandamano yalishuhudiwa katika baadhi ya maeneo nchini huku wakazi wakionyesha kutoridhishwa kwao na matokeo ya urais.
Biashara zilisimama Kisumu jioni ya Jumatatu huku waandamanaji wakimiminika barabarani kuelezea kutoridhika kwao.
The Star

William Ruto alisema alizungumza na Raila Odinga kabla ya matokeo ya uchaguzi wa urais wa Jumanne, Agosti 9, kutangazwa.
Ruto alisema bado hajazungumza na Rais Uhuru Kenyatta kuhusu maendeleo ya kisiasa akisema atafanya hivyo hivi karibuni.
Hata hivyo, alipuzilia mbali kufanya salamu za maridhiano na Raila ama washindani wake wengine, akisema yeyote anayepinga matokeo yaliyotangazwa na Chebukati aende kortini.
Ruto alisema atafanya kazi nao ili watekeleze jukumu la upinzani.

Thanks for choosing WKT. Advertise with us for affordable offers.