Huenda mshambulizi wa Manchester United, Cristiano Ronaldo, 37, akabanduka Old Trafford msimu huu na kutua Stamford Bridge kuvalia jezi ya Chelsea wanaotiwa makali na kocha Thomas Tuchel.
Kwa mujibu wa gazeti la The Atletic, mmiliki wa Chelsea, Toddy Boenly alikutana na Jorge Mendes ambaye ni wakala wa Ronaldo nchini Ureno mnamo Juni 24, 2022.
Mustakabali wa Ronaldo Old Trafford na uwezekano wake wa kuhamia Chelsea ni miongoni mwa maswala yaliyojadiliwa na wawili hao.
Licha ya Ronaldo kufungia Red Devils mabao 24 katika mechi 38 katika mashindano yote ya msimu 2021/22, Manchester United walimaliza msimu ligi nje ya mduara wa nne bora na hivyo kufeli kufuzu Champions League.
Mabingwa hao mara 20 wa EPL waliambulia nafasi ya sita na kujikatia tiketi ya kushiriki Europa League.
Ronaldo angali na miezi 12 katika mkataba wake wa miaka miwili aliotia saini mnamo Agosti 2021 alipojiunga upya na Mashetani Wekundu baada ya kuagana na Juventus ya Italia.
Chelsea wanamsaka mshambuliaji mzoefu atakaye jaza pengo la Romelu Lukaku anayewania upya na Inter Milan ya ligi kuu ya Italia almaarufu Serie A.
Tom Lutali is a seasoned scribe based in Lugari Sub-County in Kakamega County who writes human interest stories and sports for WKT.