Katika vitongoji vya mtaa wa Mareli mjini Bungoma, nakutana na Mama Irine Nanjala, ambaye ni fundi cherahani, akiwa katika shughuli zake za kila siku za kushonea wateja wake mavazi.
Kwanza nimetaka kufahamu iwapo kuna uwezekano wa mwanamke aliyetumia dawa za kupanga uzazi kupata ujauzito. Mama Nanjala ananiarifu kama mwanamke atatumia dawa hizo bila ushauri wa mhudumu wa afya, kuna uwezekano mkubwa atapata ujauzito iwapo ameshiriki tendo la ndoa bila kinga.
Vilevile iwapo mwanamke atachanganya dawa za kiasili pamoja na zile za hospitalini, kuna uwezekano mkubwa ataathiri uwezo wa dawa ya upangaji uzazi kufanya kazi mwilini.
Nasaha kutoka kwa mtaalamu
Ili kupata ufafanuzi zaidi, naabiri tuk tuk hadi hospitali ya Hopkins Crescent iliyopo Kanduyi hapa Bungoma. Nakutana na mtaalamu wa maswala ya afya ya uzazi Daktari Sarah Nekesa ambaye anafafanua zaidi usemi wa Mama Irine.
Daktari Nekesa anasema katika swala la upangaji uzazi, kuna masharti muhimu mwanamke anafaa kuzingatia na iwapo atatenda kinyume, huenda akaharibu mpango mzima.
Mtaalamu huyu, kwa mintarafu hiyo, anashauri kuwa ni muhimu mwanamke kupata maelezo kamili kutoka kwa mtaalamu wa upangaji uzazi kabla ya kuamua mbinu inayofaa mwili wake.
Nini baadhi ya athari za dawa za upangaji uzazi?
Mama Peninah Nafula Nekesa ni miongoni mwa wanawake wanaotumia mbinu za upangaji uzazi hapa Bungoma. Anakiri kuhisi maumivu ya mgongo, takribani miezi mitatu bila kupata hedhi, kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa na mwili kuwa baridi baada ya kuanza kutumia dawa hizi.
Dhana kuhusu upangaji uzazi
Swala hili limezingirwa na dhana tofauti, baadhi wakiamini kuwa iwapo mwanamke atapata ujauzito akiwa amepewa dawa ya upangaji uzazi, kuna uwezekano ajifungue mtoto mwenye ulemavu.
Mama Anastasia Ong’eti anasema alipata mimba 1999 akiwa anatumia mpango wa Nor Plant na alijifungua mtoto akiwa na afya nzuri.
Kwa hivyo anawashauri wanawake kutokuwa na wasiwasi wanapogundua wana ujauzito licha ya kuwekewa mfumo wa upangaji uzazi.
Ushirikiano wa wanandoa katika upangaji uzazi
Wataalamu wa afya ya uzazi nchini wanasisitiza ushirikiano wa wanandoa katika upangaji uzazi ili kuwa na familia yenye mpangilio.
Vilevile, wanahimiza wanaume kuwa mstari wa mbele katika swala hili zima, ikizingatiwa kuwa katika karne ya sasa, mwanamume anaweza kutumia njia ya upangaji uzazi ijulikanayo kama vasectomy.





