Magazeti ya Jumatatu, Aprili 24, 2023, yanaangazia pakubwa operesheni ya uokoaji inayoendelea katika msitu wa Shakahola, kaunti ya Kilifi, ambapo wapelelezi wamekuwa wakifukua miili iliyozikwa katika makaburi ya siri.
Daily Nation
Gazeti hili linaangazia operesheni ya ushirikiano wa idara tofauti za usalama zilizotumwa katika kaunti ya Kilifi ili kufuatilia kwa kina vifo vya kutatanisha vya waumini wa kanisa la Good News International la Pastor Paul Mackenzie.
Imeibuka sasa kuwa sio waumini wote waliokufa kwa njaa wakifuata ushauri wa mchungaji wao wa kufunga.
Polisi wanashuku kulikuwepo pia mauaji katika baadhi ya mateka baada ya kupatana na mwili wa mwanamume aliyevalia suti na tai.
Marehemu hakuonekana kuwa na dalili ya njaa kama miili mingine mingi iliyofukuliwa.
Polisi walisema wataanzisha uchunguzi kuhusu kifo cha mwanamume huyo kwa kuwa anaonekana kuwa na hali nzuri ya kiafya ikilinganishwa na wengine.
Takriban miili 39 imefukuliwa tangu wapelelezi walipoanza zoezi hilo Ijumaa, Aprili 21.
Taifa Leo
Gazeti hili linaripoti kuwa wauzaji wa pombe haramu katika eneo la Mlima Kenya sasa wanaendesha biashara hiyo katika maeneo chafu kama vile vyoo na makaburi.
Wanatumia mbinu hiyo chafu ili kukwepa kukamatwa na polisi wanaoendesha operesheni ya kumaliza biashara hiyo katika eneo hilo.
Operesheni hiyo iliamrishwa na naibu Rais Rigathi Gachagua kumaliza pombe hiyo ambayo inawaathiti vijana.
Wale wanaouza pombe ndani ya vyoo wameonekana katika kaunti za Nakuru, Nyandarua, Nyeri na Laikipia.
People Daily
Gazeti hili linaripoti kuhusu mpango wa Azimio La Umoja kurejesha tena maandamano ya kupinga serikali.
Maandamano hayo yalisitishwa muda ili kutoa fursa mazungumzo ya maridhiano yaliyoitishwa na Rais William Ruto.
Upinzani umetangaza kurejea mitaani Mei 2.
Baadhi ya masuala wanayotaka kutatuliwa ni pamoja na kupunguza gharama ya maisha, uteuzi upya wa makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na ukaguzi wa sava za tume hiyo ya uchaguzi.
The Standard
Chapisho hili linaripoti kuhusu mpango wa Ruto wa kutaka wafanyikazi wa serikali wajitolee kukatwa asimilia 3 ya mishahara yao kuchangia katika Hazina ya Nyumba.
Rais, alipokuwa akizungumza katika kanisa moja jijini Nairobi siku ya Jumapili, alisema kuna mpango wa makazi nafuu ambao serikali inawataka Wakenya wote kuchangia.
Alisema mpango huo utaanza na wafanyakazi wa serikali ambao ni takriban 700,000 kwa kukatwa asilimia 3 ya mishahara yao ili kufadhili mradi huo.
Collins Oluyali is a popular columnist who reviews the Kenyan dailies every morning in the Magazetini section, giving it a political angle with facts weaved in rich Kiswahili. Collo is also a strategist in the WKT team.