Ndivisi: Kijana auawa kwa kuibia kipofu na kutupa mali hiyo chooni
Kenya Administration Police vehicle [Photo-Courtesy]

Ndivisi: Kijana auawa kwa kuibia kipofu na kutupa mali hiyo chooni

Wenyeji wa kijiji cha Malaria katika wadi ya Ndivisi ya eneo bunge la Webuye Mashariki, Bungoma, walimpiga kitutu na kumuua kijana mmoja ambaye amekuwa akihusishwa na wizi eneo hilo.

Sambu Sanya ni kijana ambaye anasemekana amekuwa akiwakosesha wenyeji usingizi kutokana na hulka yake ya kuchukua vitu vya watu bila ruhusa.

Inakisiwa hili lilitokea baada ya kijana huyo kuingia ndani ya nyumba ya Bwana Aswani, ambaye ni mlemavu wa kutoona, na kuiba runinga na vitu vingine.

Wenyeji walipogundua kitendo hicho, walimsaka kwa muda mrefu, wakamkamata na kupata ametupa mali hiyo chooni.

Walimpata akiwa amejificha katika chumba kimoja eneo hilo kisha wakampiga kutumia vifaa butu na kumuua papo hapo.

“Huyu kijana amekuwa akisumbua wanakijiji kila mara na wananchi wamechoka na tabia yake na walikuwa wamefika mwisho ndipo wakaamua kumpiga na kumuua,” alisema Ezekiel Lusweti, mmoja wa wanakijiji.

Kijana huyo pia amehusishwa na kesi za kunajisi akina mama wakongwe na watoto wa kike eneo hilo.

“Amekuwa akitembea na kisu na akikupata anakudunga nacho na anakupora kisha kukuacha na majeraha,” Bwana Lusweti alizungumza na Western Kenya Times kupitia simu.

Maafisa wa kituo cha polisi cha Webuye walifika muda mchache baadaye na kuchukua mwili huo ambao unahifadhiwa katika hifadhi kuu ya maiti ya Webuye, kaunti ya Bungoma.

Imehaririwa na Sam Oduor
Share this article

Comments

No comments yet. Why don’t you start the discussion?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *