Maafisa wa polisi eneo bunge la Butere, kaunti ya Kakamega, wanamzuilia mwalimu mmoja kwa tuhuma za ulawiti.
Shadrak Were, mwalimu wa masomo ya Kiswahili na Kiingireza katika shule ya msingi ya Ebutayi, anaripotiwa kutumia afisi ya naibu mwalimu mkuu kufanya unyama huo.
Kulingana na wanafunzi ambao inasemekana waliwahi fanyiwa unyama huo, kila mwalimu huyo alipowadhulumu, alitishia angewaua iwapo wangemfichulia yeyote.
“Nilikuwa darasani asubuhi aliponituma kupeleka viti ofisini. Alinifuata na kunishikia kule, alizivua nguo zangu na kunifanyia unyama huo,” alisema mwanafunzi mmoja.
“Nina miaka 10 na mimi ni mwanafunzi katika darasa la nne. Siku moja mwalimu aliniita katika ofisi akafunga mlango na kunivua nguo zangu na kunifanyia uovu huo. Hii ilikuwa mara yake ya nne kunifanyia hivyo,” alisema mwanafunzi mwingine.
Wazazi sasa wanatishia kuondoa wanafunzi wao shuleni humo iwapo usimamizi wake hautachukuliwa hatua.
“Mwalimu mkuu hana haja ya kujua maslahi ya wanafunzi wake. Yeye huripoti shuleni muda mfupi tu na kuulizia pesa kabla ya kuondoka. Tutahamisha wanafunzi wetu shule iwapo hatua haitachukuliwa kwa usimamizi wa shule hiyo,” alisema mzazi mmoja.
Hata hivyo, juhudi zetu za kujaribu kupata kauli ya idara ya elimu pamoja na ile ya polisi kuhusu swala hilo hazikufua dafu kwani hakuna aliyekuwa afisini wakati tulipozuri sehemu hizo.
- Imehaririwa na Sam Oduor.
Discover the pulse of Western Kenya with WKT – your go-to digital media platform for real-time updates, rich perspectives, and powerful stories that matter.