Magazeti ya Jumatatu Januari 24, yameipa uzito makubaliano ya Naibu Rais William Ruto na kinara wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi kuungana.
Daily Nation
Gazeti hili limeangazia ndoa ya kisiasa kati ya Naibu Rais William Ruto na Mudavadi wakati wa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wa ANC lililoandaliwa katika ukumbi wa Bomas of Kenya, Nairobi, mnamo Jumapili, Januari 24.
Wakati wa mkutano huo, chama cha ANC kilimteua Mudavadi kuwa mgombeaji wake wa urais.
Wakati huo huo, Ruto, ambaye alikuwa miongoni mwa waliohudhuria, alidokeza kuhusu kuwepo kwa mpango wa kubuni ndoa ya kisiasa kati ya United Democratic Alliance (UDA) na Amani National Congress (ANC).
Ruto alisema vyama hivyo viwili vitafanya kampeni za urais pamoja kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.
“Nataka kuthibitisha kwa niaba ya UDA na timu yangu kwamba tutafanya kazi na ANC na vyama vingine vyote vinavyotaka kutembea katika safari hii ya kuleta Kenya pamoja. Kuanzia sasa tutatembea pamoja na kuanzia Jumatano, tutakuwa pamoja mjini Nakuru,” alisema Ruto.
Hata hivyo, haijabainika ni vipi muungano huo utatekeleza makubaliano yao kwani Ruto pia anawania kiti cha urais sawia na Mudavadi.
People Daily
People Daily limeangazia kuondoka kwa kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzake wa KANU Gideon Moi katika ukumbi wa Bomas.
Wawili hao walikuwa wamehudhuria mkutano wa wajumbe wa ANC siku ya Jumapili, Januari 24 wakati Mudavadi aliteuliwa rasmi kuwa mgombeaji wa urais.
Mambo yalikuwa yanakwenda sambamba hadi pale Ruto na majemedari wake walijitokeza mwendo wa saa nane mchana.
Kalonzo na Gideon waliondoka mkutano huku wakiwapungia mkono wageni waliokuwa wamehudhuia.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, KANU kilisema kiongozi wao aliondoka kwenye mkutano huo sababu “baadhi ya marafiki wa Mudavadi sio marafiki zetu na hatuko salama nao”.
Wengi walihoji kuwa kuondoka kwa wawili hao ndio mtetemeko wa ardhi uliokuwa unasubiriwa kwani hatma ya muungano wa One Kenya Alliance (OKA) sasa yayumba.
Kabla ya mkutano huo, kamati ya ushauri ya OKA ilitwikwa jukumu la kumchagua kinara wa urais wa muungano huo na ilikuwa imemfungia nje Mudavadi, hali ambayo wengi wanaamini kuwa ilimfanya aliyekuwa makamu wa rais mara moja kupoteza hamu ya muungano huo.
Uamuzi wake wa kuungana na Ruto unamaanisha kuwa yeye (Mudavadi) hana hamu ya kuwa na OKA tena anapoanza safari yake kuelekea ikulu.
Collins Oluyali is a popular columnist who reviews the Kenyan dailies every morning in the Magazetini section, giving it a political angle with facts weaved in rich Kiswahili. Collo is also a strategist in the WKT team.